OUR

KISWAHILI KIDATO CHA KWANZA: Mada: KAMUSI



Somo la leo tarehe 27/04/2020
Na
Mwl. Isaack Manase Mtalambilwa
Simu: 0768 740 225
Dodoma mjini.
Mada: KAMUSI


KAMUSI YA LUGHA; MAANA, AINA, TAARIFA NA DHIMA ZAKE.

MAANA YA KAMUSI
Massamba (2012:24) kamusi ni kitabu cha orodha ya maneno katika lugha, yaliyopangwa kwa utaratibu maalum, pamoja na maana au fasili zake; katika uchanganuzi wa lugha haya ni maneno ya kileksika, yaani yasiyokuwa ya kisarufi au kifonolija.
Tuki (1990:21) kamusi ni kitabu cha orodha ya maneno yaliyopangwa kwa utaratibu maalum, pamoja na maana na fasili zake.
Wamitila (2003:76) kamusi ni kitabu ambacho kina orodha ya maneno katika lugha Fulani ana ambayo hupangwa ki-abjadi au kialfabeti. Maneno haya huelezewa maana zake mbalimbali na labda hata vyanzo vyake.
Kwa ujumla  kamusi ni kitabu chenye orodha ya maneno mbalimbali yaliyopangwa vizuri kwa kufuata alfabeti na hutoa taarifa mbalimbali kama vile maana, matamshi n.k.

MUUNDO WA KAMUSI
i)  Utangulizi wa Kamusi
Hii ni sehemu ya mwanzo ambayo hutangulia matini yenyewe ya kamusi.
ii)  Matini ya Kamusi
Hii ni sehemu ambayo inaonyesha vidahizo na fahiwa zake kuanzia herufi A-Z.
iii)  Sherehe ya Kamusi
hizi ni baadhi ya taarifa ambazo huwa zimeandikwa mwishoni mwa kamusi. Kwa mfano majina ya nchi, lugha za mataifa duniani, vipimo vya urefu, vipimo vya uzito, ujazo  n.k.

AINA ZA KAMUSI
Kwa kutumia kigezo cha LUGHA kuna aina kuu tatu (3) za kamusi
i) kamusi wahidiya
hii ni kamusi inayoandikwa kwa lugha moja
ii) kamusi thaniya
Hii ni kamusi inayoandikwa kwa lugha mbili.
iii) kamusi mahuluti
Hii ni kamusi inayoandikwa kwa lugha zaidi ya mbili. Kwa mfano Kiswahili-kiingereza-kifaransa.

Taaarifa zinazopatikana katika kamusi
Taarifa hizi huweza kuwa za kisarufi au kileksika
a) taarifa za kisarufi zinazoingizwa katika kamusi.
Nyambari na Masebo (2012:184) wameainisha taarifa zifutazo za kisarufi zinazopatikana katika kamusi.
       Wingi wa nomino
       Kategoria ya kisarufi ya kidahizo mf. Kitenzi (kt), nomino (nm) n.k
       Vinyumbuo vya vitenzi mf. Piga-pigwa-pigana-pigika n.k
       Ngeli za nomino mf. Mtu (A-YU), kazi (i-)
       Matamshi ya neno
       Elekezi au sielekezi. Mfano: Apiza kt  [ele], Anguka kt  [sie]
       Mifano ya matumizi

b) Taarifa za kileksia zinazopatikana katika kamusi
       Mpangilio wa vidahizo
       Kategoria za maneno
       Umoja na wingi
       Upatanisho wa kisarufi
       Uelekezi wa vitenzi
       Maana ya vidahizo
       Tahajia za maneno
       Mifano ya matumizi
       Methali, nahau na misemo
       Timolojia ya leksimu
       Michoro/ picha
       Matamshi


DHIMA ZA KAMUSI
       Huonesha tahajia sahihi za maneno
       Huonesha maana za maneno
       Huonesha matamshi sahihi ya maneno
       Huonesha asili ya neno
       Humsaidia mtumiaji kujifunza lugha za kigeni
       Huonesha alama na vifupisho mbalimbali katika lugha husika.


                   KAZI YA KUFANYA
1. Taja faida 5 za kamusi.





 Marejeleo
Massamba. D.P.B.(2004 ). Kamusi ya isimu na falsafa ya lugha. Dares salaam: TUKI
TUKI (1990).kamusi sanifu ya isimu na lugha. Dares salaam: Tuki na Educational publishers and distributors ltd.
Wamitila. K. W. (2003). Kamusi ya fasihi, istilahi na nadharia. Nairobi: Focus publishers ltd.

CORONA (COVID 19) INAUA: TUFATE USHAURI WA WATAALAMU NA SERIKALI KUJIKINGA
BAKI NYUMBANI, UBAKI SALAMA


No comments:

Post a Comment

Pages